Tanzania ipo imara usalama mtandaoni

ARUSHA-Tanzania imeendelea kushikilia rekodi ya ubora duniani katika viwango vya usimamizi wa hali ya juu vya usalama mitandaoni.
Hayo yamesemwa leo Aprili 10,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga katika siku ya kwanza ya Jukwaa la Nne la Usalama Mtandaoni (Tanzania Cyber Security Forum 2025) linaloendelea katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Amesema, kwa mujibu wa ripoti ya Usalama Mtandaoni (Global Cybersecurity Index (GCI) ya mwaka 2024 iliyotolewa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU),Tanzania imewekwa katika Kundi la 1 (Tier 1), ambayo ni ngazi ya juu zaidi duniani kwa ubora wa usalama mtandaoni. "Duniani kote ni nchi 46 tu zenye hadhi hii."
Amesema,ripoti hiyo inaonesha Tanzania kuwa na viwango vya juu vya mfano katika ufanisi wa kusimamia nguzo tano za usalama mitandaoni ziliyowekwa na ITU kuanzia mwaka 2015.

Hatua hiyo amesema, imetokana na vipimo vya GCI kubaini Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya kisheria kuhusu usalama mtandaoni.

Pia, ripoti hiyo ilibaini Tanzania imepiga hatua kubwa kwa upande wa mikakati na mipango ya kiufundi, kiutawala, uendeshaji wa mifumo, kujenga uwezo na ushirikiano katika masuala yanayohusu usalama mtandaoni.
Kuhusiana na jukwaa hilo, Dkt.Mwasaga amesema kuwa, ni jukwaa muhimu ambalo limewakutanisha wadau muhimu kutoka serikalini, sekta binafsi, vyuo vikuu, asasi za kiraia na washirika wa kimataifa kwa lengo la kushirikiana, kubadilishana maarifa, na kujengeana uwezo.

Pia, amesema jukwaa hilo la siku mbili linaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Kuimarisha Uimara na Kukabiliana na Vitisho Katika Uchumi wa Kidijitali".

Vilevile, Dkt.Mwasaga amesema, jukwaa hilo linajumuisha mijadala ya wataalamu, warsha za kiufundi, mijadala ya kisera, fursa za kujenga mtandao wa ushirikiano, pamoja na mafunzo ya vitendo yenye lengo la kuimarisha uimara wa Tanzania dhidi ya matishio ya usalama mtandaoni.

Dkt.Mwasaga amesema, miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya mtandao endelevu na jumuishi, kuendeleza uimara wa sekta muhimu.

Mada nyingine, Dkt.Mwasaga amesema, itaangazia juu ya namna ya kulinda mtandao katika enzi ya teknolojia zinazoibuka na nyingine ni namna ya kutumia mtandao kama injini ya ukuaji wa uchumi.
Wakati huo huo, Dkt.Mwasaga amesema, Tanzania ina nguzo tazo za mabadiliko ya kidijitali ambazo zinajikita katika ujuzi wa kidijitali,usalama wa kidijitali na uaminifu.

"Nguzo ya pili inahusiana na usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, na ulinzi wa watumiaji katika uchumi wa kidijitali."

Nguzo nyingine ni huduma za mawasiliano ya kidijitali,uchumi wa kidijitali, utafiti wa kidijitali,ubunifu na ujasiriamali.
Dkt.Mwasaga amesema,katika jukwaa la tatu la Usalama wa Mitandaoni nchini ambalo lilifanyika Aprili 4 hadi 5,2024 katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha walitoka na maazimio kadhaa.

Miongoni mwa maazimio hayo, Dkt.Mwasaga amesema yalikuwa ni;

a) Kuongeza uelewa kwa umma kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi

b) Kuhamasisha ushiriki wa wataalamu wa usalama wa mtandao katika mabadiliko ya kidijitali

c) Kusaidia ubunifu wa ndani na suluhisho katika usalama wa mtandao

d) Kupitia sheria za usalama wa mtandao ili kujumuisha wataalamu wa ndani

e) Kutambua wataalamu waliothibitishwa na Tume ya TEHAMA

f) Kuwekeza zaidi kwenye kukuza uwezo wa ndani katika usalama wa mtandao

g) Kukuza makampuni ya ndani yanayotoa huduma za usalama wa mtandao

h) Kuweka suluhisho katika kitambulisho cha kidijitali.

i) Kuanzisha bima ya usalama wa mtandao ili kupunguza hasara za kifedha

j) Kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika elimu ya usalama wa mtandao

k) Kutambua usalama wa mtandao kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi

l) Kuwakutanisha wadau muhimu katika mijadala ya baadaye kuhusu mtandao

Changamoto

Dkt.Mwasaga akizungumzia kuhusu changamoto za Kimataifa za kiusalama mtandaoni amesema, kwa mujibu wa ITU, changamoto kubwa ni kuongezeka kwa programu hasidi (ransomware).
Changamoto nyingine ni matukio ya wizi wa taarifa (data) katika sekta nyeti kama elimu, nishati na uzalishaji.

Dkt.Mwasaga amesema, nyingine ni ukiukwaji wa faragha ambapo Ulaya pekee ilitoza faini zaidi ya Euro bilioni 1.9 mwaka 2023.

Pia, kuna suala la gharama kubwa katika biashara ambapo wastani wa gharama ya wizi wa data ilikuwa dola za kimarekani milioni 4.45 mwaka 2023 ikiwemo hitilafu za mfumo zinazoathiri huduma na minyororo ya usambazaji.
Amesema,kadri uhalifu wa kimtandao unavyozidi kuongezeka, ni muhimu kwa biashara, taasisi za serikali, na watu binafsi kuchukua hatua za mapema za kujilinda dhidi ya vitisho hivyo na kulinda taarifa nyeti pamoja na miundombinu yake muhimu.

Jukwaa hili linaendana na Dira ya Tanzania ya kuwa na Uchumi wa Kidijitali ulio salama na wenye mafanikio.

International news

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post