SONGWE-Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa mashamba kwa wakulima waliosajiliwa mkoani Songwe aliposhiriki kwenye zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima wa Kijiji cha Kanga kilichopo katika Wilaya ya Songwe mkoani Songwe.
Wakulima wa kijiji cha Kanga wakiendelea kuweka saini kwenye hati zao ikiwa ni hatua ya sita ya zoezi la kumilikishwa ardhi kisheria baada ya kuhakiki taarifa zao kabla ya kuzichukua rasmi.
Laurent ameonesha kuridhishwa na zoezi hilo leo tarehe Mosi Aprili, 2025 alipotembelea kijiji hicho kujionea utekelezaji wa zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima 3,098 wa vijiji vya Gua, Kapalala, Kanga na Galula linalotekelezwa kwa awamu ya kwanza katika wilaya ya Songwe kwa ushirikiano baina ya TFRA, NLUPC na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.
Zoezi hilo linaenda sambamba na uhuishaji na usajili wa wakulima, uchukuaji wa taarifa kwa ajili ya upatikanaji wa kadi janja na uandikishaji wa wakulima kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa (NIDA).




Aidha Bw. Laurent amewahakikishia wakulima kuwa ni nia ya serikali kuhakikisha wakulima waliosajiliwa na kukidhi vigezo wanapatiwa hati miliki na kadi janja za utambulisho wa mkulima.
Hatua ambayo itamsaidia mkulima kunufaika na umiliki wa ardhi na fursa mbalimbali zikiwemo za kifedha na mikopo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC katika tukio hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa, amesema Ukamilishaji wa hatuaya sita ya uandaaji wa mipango ya Matumizi ya Ardhi ni muhimu kwni inahusisha utoaji wa hati za Hakimiliki za Kimila zinazowawezesha wakulima kuongeza usalam wa ardhi zao.
Aidha,Kishoa ameongeza kuwa, utekelezaji wa hatua hii utaiwezesha TFRA kupata taarifa sahihi za mashamba ya wakulima ili kuboresha utoaji wa huduma za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu kwa bei ya ruzuku .
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kanga, Mhe. Erick Kihinda, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele wakulima wa Mkoa wa Songwe kupimiwa mashamba yao na kupewa hati miliki zitakazowafaa katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususan katika kuendeleza kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo alizeti, mahindi na ufuta.
“Serikali imewamilikishia wakulima ardhi zao bure, jambo hili ni la kushukuru sana,” amesema. Hati hizi zitasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kuwapa wakulima nafasi ya kupata mikopo ili kuboresha kilimo chao”. Kihinda alimaliza.
Afisa tarafa wa Tarafa ya Songwe, Godwin Kaunda, akizungumza na wakulima wa kijiji cha Kanga kilichopo Wilaya ya Songwe mkoani Songwe waliofika kwa ajili ya kuhakiki taarifa za hati miliki za mashamba tukio lilifanyika kwenye ofisi za kijiji tarehe 1 Aprili, 2025.
Naye, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Songwe, Godwin Kaunda, amesema serikali inatekeleza majukumu yake kwa wakati kama inavyoahidi.
“Ni mwaka jana tu tulianza zoezi la upimaji wa mashamba lakini leo tunakwenda kuhakiki hati zetu. Urasimishaji wa ardhi unaleta usalama kwa wakulima na kusaidia kuondoa migogoro ya mipaka iliyokuwepo hapo awali’’, amesema Kaunda.