DODOMA-Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde amekutana na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kujadiliana juu ya maendeleo ya sekta ya madini nchini na hasa uendelezaji wa madini mkakati.

Jumuiya ya Ulaya imeonesha utayari wa kuunga mkono jitihada kubwa za kuendeleza sekta ya madini nchini kwa kutenga kiasi cha euro 60 milioni ambayo itaelekezwa katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo ujenzi wa miundombimbu ya barabara kwa maeneo ya uchimbaji,upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika,kuwajengea uwezo watanzania kupitia mafunzo ya ufundi na kufanya utafiti wa kina wa madini katika maeneo mbalimbali chini.


“Kipaumbele kikubwa kwa sasa nchini kwetu ni kuona madini yetu yanaongezwa thamani nchini ili tuweze kupata manufaa zaidi.
Hivyo ushirikiano wetu pia lazima uliangalie kwa kipekee hili eneo kwa kuvutia uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani nchini,”alisema Mavunde.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Taaisisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini (GST),Dkt. Musa Budeba na Kamishna Msaidizi wa Madini,Eng.Terence Ngole.