Urekebu wa Sheria una manufaa makubwa nchini-Mwanasheria Mkuu wa Serikali

DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza Johari amesema, Urekebu wa Sheria ni mradi ambao Serikali kupitia ofisi yake inaufanya kwa lengo la kujumuisha marekebisho mbalimbali ya sheria yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwa kitu kimoja.
“Urekebu wa Sheria ni mradi ambao Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaufanya kwa lengo la kujumuisha yale marekebisho mbalimbali ya sheria yaliyofanywa na Bunge kuwa kitu kimoja.

"Kwa sababu unapokuwa na sheria mama iliyotungwa awali halafu kuna sheria ya marekebisho inayohusu sheria hiyo inampa ugumu kidogo mtumiaji kwa maana atahitaji kusoma sheria mama, lakini akasome na ile ya mjumuisho;

Ameyasema hayo leo Aprili 22, 2025 wakati wa mahojiano katika Kipindi cha Jambo Tanzania cha runinga ya Taifa ya TBC1jijini Dodoma.

Pia,amesema wakati mwingine mtumiajia anaweza asifahamu kama kuna marekebisho ya sheria mama, hivyo kutokana na changamoto hiyo ndipo urekebu wa sheria hufanyika.

Ameongeza kuwa, ofisi yake ipo pamoja na wananchi katika kuhakikisha inawapa ushauri stahiki katika changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na inasaidia kutatua changamoto hizo kupitia kliniki za sheria.

Mheshimiwa Johari amesema hadi sasa zaidi ya wananchi 1,000 wameshafikiwa ambapo mawakili kutoka ofisi yake wanatoa huduma hizo na kwamba kwa mwezi Mei,mwaka huu kliniki ya sheria itafanyika mkoani Singida baada ya kumaliza ratiba yake mkoani Mwanza.

“Tunapokea malalamiko mbalimbali ya wananchi, na sisi kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jukumu letu ni kutatua malalamiko mbalimbali ya wananchi na tunalifanya hilo kupitia utaratibu ambao tumeuanzisha, tuna kliniki za sheria ambazo tunazifanya katika mikoa mbalimbali."

Amesema,wanachokifanya katika wiki husika wanapokuwa kwenye mkoa husika wanakuwa hapo kwa siku saba wakiwa na mabanda yao.

"Katika kliniki hizo tunapokea malalamiko mbalimbali ya wananchi na tunawapa ushauri mbalimbali, mengine tunayatatua na mengine tunaendelea kuyafuatilia, tumekuwa tukifanya hivyo."

Miongoni mwa malalamiko ambayo wamekuwa wakiyapokea kutoka kwa wananchi na kuyashughulikia, Mheshimiwa Johari amesema ni yale yanayohusu ardhi,mirathi na ndoa.

Amesema kuwa,ofisi yake inapokutana na changamoto hizo inasaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma ya utatuzi na pia kutoa elimu kwa wananchi.

Tazama sehemu ya mahojiano hapa;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news