Wadau wa ununuzi wahimizwa kuzingatia maadili kazini

ARUSHA-Wadau wa Ununuzi waaswa kuzingatia maadili na elimu katika Ununuzi wa Umma ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha.
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando akiongea na wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali (hawapo pichani) kwa Kanda ya Kaskazini.

Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kuhusu matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST) kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika jijini Arusha.

Bw. Sando amesema kuwa baadhi ya kesi zinazowasilishwa PPAA kwa asilimia kubwa zinakuwa zimesababishwa na ukiukwaji wa maadili.
Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Bi. Florida Mapunda akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Kaskazini jijini Arusha.

“Kama wadau katika sekta ya ununuzi wa umma ni muhimu sana kuzingatia maadili kwa sababu ndiyo itakayoipatia serikali thamani halisi ya fedha na heshima, sote tunajua mifumo ya ununuzi ipo lakini inaongozwa na binadamu kama hawana maadili mifumo haina maana,” alisema Bw. Sando.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST akifafanua jambo wakati wa mafunzo yaliyofanyika jijini Arusha.

Bw. Sando aliongeza kuwa unaweza kutengeneza sheria nzuri sana lakini kama watu hawataamua kuwa watiifu wa sheria hiyo kutakuwa na uvunjifu mkubwa wa sheria katika nchini hiyo.

“...vivyo hivyo hata sisi tukikosa maadili katika sekta ya ununuzi wa umma tutakuwa na kesi nyingi sana,kutakuwa na upotevu wa fedha za umma,”aliongeza Bw.Sando.

Kadhalika, Bw. Sando amewataka washiriki walipota fursa ya kuhudhuria mfunzo hayo kwa Kanda ya Kaskazini kuwaelimisha wadau wengine kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).Naye mmoja wa wadau wa ununuzi wa umma aliyeshiriki mafunzo hayo Bi. Rachel Werema aliipongeza PPAA kwa kuandaa mafunzo hayo ya siku mbili kwani yamewasaidia kufahamu namna ya kuwasilisha malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya ununuzi kwa wakati kupitia moduli iliyopo katika mfumo wa NeST.

Mafunzo hayo ya siku mbili kwa Kanda ya Kaskazini yelifanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 10 – 11 Aprili, 2025 yalihudhuriwa na washiriki 240 kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

Awamu ya kwanza ya mafunzo kikanda yalifanyika Kanda ya Ziwa kwa siku tatu ambapo yalijumuisha washiriki zaidi ya 580 mkoani Mwanza kuanzia tarehe 4 – 6 Februari, 2025 yakijumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news