ARUSHA-Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela (The Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST) imezindua kituo maalum cha utafiti wa teknolojia za kisasa kwa ufugaji fanisi kinacholenga kutatua changamoto za ufuguji wa ng’ombe wa maziwa ikiwemo kutoa taarifa ya maradhi, chakula na muda sahihi wa joto kwa ajili kupandikiza.
Akizungumza wakati wa kuzindua kituo hicho Aprili 11, 2025 katika kampasi ya Tengeru, jijini Arusha, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula, ameeleza kuwa, kazi kubwa ya taasisi hiyo ni kuzalisha teknolojia mpya pamoja na kuhuisha zilizopo lengo likiwa ni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii pamoja na viwanda.
“Kituo hiki kitawezesha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kujifunza kwa kina namna ya kutumia teknolojia ya kisasa kupitia kifaa maalum cha donge kitakachowekwa kwenye tumbo la ng'ombe ili kujua kiasi sahihi cha chakula, maji na muda sahihi kupanda kwa joto kwa ajili ya upandikizaji," Prof. Kipanyula.

Aidha,Prof. Kipanyula ameleza kuwa, kifaa hicho baada ya kuwekwa kwa mnyama hufungwa katika banda na kuunganisha mawasiliano katika simu hivyo kumuwezesha mfugaji kutembea na mifugo yake kiganjani kwa kupata taarifa muhimu zinazosaidia kujua na kutekeleza uhitaji kwa wakati.
"Teknolojia hii itasaidia kuondokana na changamoto ya kukisia kuhusu ulaji, unywaji na upandishaji joto kwa ng'ombe, jambo ambalo litaongeza uzalishaji wa maziwa pamoja na ndama,"anasema Prof. Kipanyula.
Kwa takwimu ng'ombe anatakiwa kupata ndama kila mwaka lakini kutokana na changamoto ya ulishaji na kupata taarifa kwa wakati kuhusu kupandishwa kwa joto la mnyama, wafugaji wamekuwa wakipata ndama kila baada ya miaka miwili hadi mitatu jambo ambalo linadunisha uzalishaji.

“Kituo kitajikita katika kufanya utafiti, kutambua aina ya mifugo na ulishaji wake, kutambua ng’ombe akiwa ameingia joto kwa wakati, unywaji wa maji kwa mnyama, kuendeleza, kupima na kuhuisha teknolojia zilizopo pamoja na kutoa mafunzo kwa wafugaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,"amesisitiza Prof. Shirima.