PWANI-Serikali inaendelea na utekelezaji wa mkakati wake wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa zinazotumika migodini na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

"Mh. Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kufungua fursa na kuweka mazingira mazuri yanayovutia uwekezaji nchini. Matokeo ya kazi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda hiki cha kuzalisha bidhaa hizi ambazo ni muhimu sana kwenye uchimbaji wa madini.

Matumizi ya baruti nchini ni tani 26,000 na vilipuzi pisi milioni 10 kwa mwaka, hivyo ujio wa kiwanda hichi kitakachozalisha tani 22,000 za baruti na vilipuzi pisi milioni 15 utasaidia kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi na kuuza katika nchi zinazotuzunguka.
Uzalishaji wa baruti na vilipuzi ndani ya nchi utasaidia kupunguza gharama ya bidhaa hiyo kwa wachimbaji, ajira kwa wananchi na kuongeza ujuzi na elimu kwa watanzania.
Awali, Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Solar Nitrochemicals Limited, Bw. Kishor Bhomale alieleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umegarimu Dola za Kimarekani Milioni 8 Sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 19 na wamelenga kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mheshimiwa Petro Magoti alieleza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utachochea ukuaji wa kiuchumi wa Kisarawe na pia wametenga eneo kubwa kwa ajili ya viwanda na kwamba wapo tayari kupokea wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.