DODOMA-Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Deogratius Ndejembi amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka za kuvunja nyumba iliyojengwa katika kiwanja kikichovamiwa eneo la Iyumbu North mkoani Dodoma.

“Msimamizi wa mirathi alituletea taarifa ya kuvamiwa eneo hili na mvamizi ameaanza ujenzi katika kiwanja chao ambacho ni 1/31 licha ya jitihada za kumsimamisha katika ujenzi huo tangu anajenga msingi, lakini ameendelea kujenga hadi kupaua mpaka amepiga plasta na kufunga madirisha. Lakini hana kibali cha ujenzi katika kiwanja hiki na wala si mmiliki halali wa kiwanja hiki,” amesema Waziri Ndejembi.

Aidha, Waziri Ndejembi ametoa rai kwa watu kuacha kuvamia maeneo ya watu wengine ambayo yana umiliki na nyaraka halali katika jiji la Dodoma na maeneo mengine nchini.
Kwa upande wake msimamizi wa mirathi,Bi. Prisca Lukas Lulambo amesema kuwa, aligundua eneo hilo limevamia mwaka 2021 na mvamizi Geogre Beno Mlonge na alipoenda kujiridhisha ofisi za jiji juu ya umiliki wake alijulishwa kuwa umiliki wa kiwanja hicho ni wa Thobias Simon Msigwa.