ARUSHA-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amelitaka Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kuongeza jitihada katika usimamizi na kuhakikisha malengo ya chuo ya muda mrefu na muda mfupi yanafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Waziri Riziki ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza jipya la Uongozi wa Chuo hicho iliyofanyika katika Ukumbi wa IAA, Arusha.

Amesema Chuo cha Uhasibu Arusha kimeamua kujitofautisha na vyuo vingine kwa namna mbalimbali ikiwemo kuanzisha mitaala ya kipekee mfano mitaala ya uanagenzi (apprenticeship), kuanzisha mitaala inayoandaa wataalam wanaoweza kujiajiri na kuajiri wengine, kutengeneza miundombinu na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Hivyo ametoa rai kwa Baraza hilo kuhimiza juhudi za kuboresha ubora wa elimu inayotolewa na chuo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mitaala itakayoanzishwa katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yao ili inaendelea kuwa mfano katika kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kutoa wasomi watakao ongeza nguvu katika kutatua changamoto katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Mhe Riziki amefahamisha Baraza la Uongozi ni chombo muhimu katika kuhakikisha usimamizi bora wa shughuli za chuo, kuimarisha utawala bora, na kusimamia utekelezaji wa mikakati inayolenga kuboresha elimu na huduma zinazotolewa na chuo.
Aidha amewakumbusha umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji, na ushirikishwaji wa wadau wote kwani itasaidia kujenga mazingira ya kuaminiana na kushirikiana kwa karibu katika kufanikisha malengo ya chuo chao.
Sambamba na hayo Mhe.Riziki amewataka kuhakikisha wanasimamia maadili na misingi imara na uwajibikaji kwa menejimenti na Wanafunzi kwa ujumla ili kuona Taifa la Tanzania linaendelea kusimamiwa vizuri.

Vile vile Mhe. Riziki amewapongeza wajumbe wapya kwa kuteuliwa kuwa sehemu ya Baraza hilo la Uongozi ambapo amesema uteuzi wao ni ishara ya imani kubwa ya Serikali na wananchi. Hivyo amewataka kutumia ujuzi na uzoefu wao katika kushauri na kusimamia mambo mbalimbali ya Chuo kwa manufaa ya Wanafunzi, Wafanyakazi, na jamii kwa ujumla.
Mhe.Riziki ametumia fursa hiyo kuwaomba kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kuhubiri amani ya nchi na kuunga mkono juhudi za viongozi wakuu wa nchi Dr. Samia Suluhu Hassan na Dr. Hussein Mwinyi katika kuona wanalinda na kuisimamia amani ya nchi na maendeleo kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka, ameelezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuwa ni pamoja na Ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika Kampasi za Arusha, Babati, Dodoma na kuanza kwa hatua za ujenzi katika Kampasi ya Songea pamoja na ongezeko la mitaala, Wanafunzi na Wafanyakazi.
Akitoa shukurani zake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli amemuhakikishia Mhe.Riziki kuwa, wataendelea kusimamia maadili na uwajibikaji katika chuo hicho ili malengo yaweze kufikiwa, huku akimshukuru Mhe.Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa Kuendelea kumuamini kuongoza kwenye nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa awamu ya pili.

Baraza la chuo cha Uhasibu Arusha limezinduliwa rasmi tarehe 8/04/2025 likiwa na wajumbe 12, na litafanya kazi zake kwa muda wa miaka mitatu.