NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema kuwa, tathmini inaonesha wananchi wengi wameridhishwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuondoa zuio la mabasi kusafiri usiku.
Hayo yamesemwa leo Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),CPA Habibu Suluo katika kikao kazi na wahariri, waandishi wa habari nchini,chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
CPA Suluo amesema, wamefanya tathmini tangu kuanza kutoa vibali vya mabasi kusafiri usiku ambayo imeonesha namna ambavyo wananchi wanafurahia huduma hiyo.
"Sisi (LATRA) tuna kitengo cha udhibiti uchumi ambacho kinafanya tafiti, tathmini ya LATRA ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa ruhusa hii ya safari za usiku na mchana (24/7) umeonesha wananchi wengi wamefurahishwa na kuridhishwa na maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mabasi kusafiri usiku."
Aidha, amesema kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kutumia usafiri wa usiku kuliko mchana na msongamano wa abiria kwenye stendi umepungua sana.
"Na mchezo wa mabasi kukimbizana umepungua sana na unaelekea kwisha kabisa. Vilevile,tathmini ya LATRA inaonesha kuwa safari hizi za 24/7 zimepunguza gharama za njiani kwa abiria na kuboresha matumizi ya muda wao kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na kujiongezea vipato.
"Ninyi wahariri na wanahabari ni mashahidi na kama hamjafurahia itakuwa ni jambo la ajabu."
CPA Suluo amesema,Serikali ya Awamu ya Sita iliondoa zuio la mabasi ya abiria kusafiri nyakati za usiku lililowekwa mwaka 1994.
Juni 28,2023 akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) aliziagiza, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchina Wizara ya Uchukuzi kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa mabasi nyakati za usiku.
Amesema, LATRA ilishiriki katika zoezi la kufanya maandalizi ya kuanza kwa safari za usiku kwa kushirikiana na wadau wake muhimu hasa wamiliki wa mabasi wakiwemo TABOA.
Pia,ilitekeleza maamuzi ya Serikali kwa kuanza kutoa ratiba za mabasi kusafiri usiku na mchana (24/7) kuanzia Oktoba 1,2023.
Septemba 29, 2023, akitangaza kwa niaba ya Serikali kuanza kwa ratiba za safari za usiku, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Jumanne Sagini (Mb) alieleza sababu sita za Serikali kuruhusu safari za usiku.
Miongoni mwa sababu hizo ni udhibiti wa usalama kupitia Jeshi la Polisi kuimarishwa kutokana na jitihada za Serikali ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sababu nyingine ni mwamko wa wananchi, hususan wafanyabiashara kutumia taasisi za kifedha badala ya kusafiri na fedha taslimu (cash) kuongezeka.
Pia,Serikali imeimarisha huduma za mawasiliano ya simu kwa kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo mengi nchini.
Vilevile,Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inao Mfumo madhubuti wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) unaofanya kazi kwa saa 24.
Aidha,Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeboresha miundombinu ya usafiri, hususan barabara kuu na barabara za mikoa na hivyo kufanya nchi yetu kuwa moja ya nchi zenye usafiri wa barabara unaoaminika na bora.
Sababu nyingine ilikuwa ni wafanyabiashara wengi wanaomiliki mabasi ya abiria walio tayari kufanya safari za saa 24 na wako tayari pia kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo kuhusu usafiri na usafirishaji wa abiria.
CPA Suluo ameeleza kuwa,tangu kuanza kwa huduma za usafiri wa 24/7, LATRA imeendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani katika uratibu wa huduma za usafiri wa mabasi kwa kuimarisha usimamizi wa masharti ya leseni ikiwemo ukaguzi wa mabasi, utambuzi wa madereva kwa i-buttons na matumizi ya VTS.
Amesema, hadi kufikia Machi 31,2025 mabasi 2,323 yalikuwa yamepatiwa ratiba za kutoa huduma za usafiri usiku na mchana (24/7).