Yote haya yanatokana na upendo wa Rais Dkt.Samia kwa Watanzania-Kadogosa

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw.Masanja Kadogosa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliamini shirika hilo na kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza miradi ya ukarabati wa miundombinu ya reli iliyopo na ujenzi wa miundombinu mipya ya SGR.
Amesema, tangu Rais Dkt.Samia aingie madarakani amekuwa mstari wa mbele kutekeleza miradi yote ikiwemo ile ya kimkakati, jambo ambalo si rahisi kufanywa na mtu yeyote.

Kadogosa amesema kuwa, mara nyingi viongozi wapya wanapoingia madarakani, huwa na mikakati yao na si rahisi kutekeleza miradi walioikuta katikati au iliyokuwa katika hatua za utekelezaji, lakini kwa Rais Dkt.Samia ameonesha upendo wa hali ya juu kwa Watanzania.

Ni kupitia miradi ya reli ambayo amesema, Rais Dkt.Samia ameipa kipaumbele cha kipekee ikizingatiwa kuwa, ina faida nyingi ikiwemo kukuza ajira, kupunguza msongamano wa magari, kubeba mizigo mingi kwa wakati mmoja, kulinda mazingira na kuchangia katika pato la Taifa.

Kutokana na upendo huo wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa Watanzania, Kadogosa amesema kuwa,utekelezaji wa Mradi wa SGR unaendelea katika awamu mbili ambapo jumla ya mikataba iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji ina thamani ya shilingi trilioni 29.580.

Kadogosa ameyasema hayo leo Aprili 3,2025 mkoani Morogoro wakati akitoa wasilisho katika kikao kazi cha pamoja baina ya Menejimenti ya TRC na wanahabari wa mitandao ya jamii.Kikao kazi hicho kinalenga kutoa elimu, maarifa na stadi za namna bora ya kuripoti habari za Reli nchini.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Kadogosa amesema kuwa,Lot 1 ambayo inajumuisha kipande cha reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 hadi kufikia Februari,2025 utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 99.68.

Kuhusu Lot 2 ambayo inajumuisha kipande cha reli kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 utekelezaji wake umefikia asilimia 97.85 hadi kufikia Februari,2025.

Vilevile, katika awamu hiyo ya kwanza, kuhusu Lot 3 ambayo inajumuisha kipande cha Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilomita 368, Kadogosa amesema, utekelezaji wake umefikia asilimia 14.53.

Kwa upande wa Lot 4 ambayo inajumuisha kipande cha Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilomita 165,Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC amesema, utekelezaji wake umefikia asilimia 6.61.

Upande wa Lot 5 ambao unajumuisha kipande cha Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilomita 341, amesema kuwa, utekelezaji wake umefikia asilimia 63.10.

Aidha, kwa upande wa awamu ya pili ambao una Lot 6 inayojumuisha kipande cha Tabora hadi Kigoma chenye urefu wa kilomita 506, utekelezaji wake umefikia asilimia 7.81.

Katika hiyo awamu ya pili pia, Kadogosa amesema,Lot 7 ambayo inajumuisha kipande cha Uvinza hadi Malagarasi chenye urefu wa kilomita 180 mkataba ulisainiwa Januari 29,mwaka huu ikiwemo Lot 8 inayohusisha kipande cha Malagarasi hadi Musongati chenye urefu wa kilomita 102 ambapo utekelezaji wake unaanza.

Mbali na hayo, Kadogosa amesema, shirika hilo linaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ambayo kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ujenzi huo ni pamoja na reli ya Mtwara-Songea hadi Mbamba-Bay na Matawi, Liganga hadi Mchuchuma yenye urefu wa kilomita 1,000.

"Tayari upembuzi na usanifu wa awali umekamilika, na sasa tupo kwenye hatua za utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli, kwa kushirikisha sekta binafsi (PPP)."

Pia, amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na wabia wkae wameonesha utayari wa kuunga mkono mradi huo wa kimkakati kwa upande wa Ushoroba wa Kusini kwa nchi za Tanzania,Msumbiji, Zambia na Malawi.

Kuhusu ujenzi wa reli ya Tanga,Arusha hadi Musoma mkoani Mara yenye urefu wa kilomita 1,053, Kadogosa amesema,usanifu wa awali na upembuzi yakinifu umekamilika ambapo pia, hatua za utafutaji wa fedha za ujenzi zinaendelea kwa kushirikiana na sekta binafsi.

"Ujenzi wa reli ya Kaliua, Mpanda hadi Karema yenye urefu wa kilomita 317, upande wa ujenzi wa SGR, usanifu wa awali upembuzi yakinifu umekamilika na hatua za utafutaji wa fedha za ujenzi zinaendelea."

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa,pia uboreshaji wa miundombinu ya reli ya kati (MGR) unaendelea kati ya Kaliua na Mpanda.

Burundi

Wakati huo huo, Kadogosa amesema kuwa, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Tanzania katika uwekezaji kwenye Reli, Serikali ya Burundi imeridhia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kusimamia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Kigoma hadi Burundi kutokana na uzoefu katika utekelezaji wa mradi kama huo nchini. 

Pia, amesema TRC imepata uzoefu na imeendelea kupokea na kutoa ushauri wa kibobezi kwa nchi zingine Afrika Jamhuri ya Uganda,Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ikumbukwe kuwa, TRC ni miongoni mwa smwa mashirika ya umma nchini ambalo lilianzishwa chini ya Sheria ya Reli Na.10 ya mwaka 2017 ambapo lipo chini ya Wizarta ya Uchukuzi.

Dira ya TRC ni kuwa mtoa huduma za usafiri wa reli wenye ufanisi na wa kuaminika barani Afrika na lina wajibu wa kuendeleza miundombinu ya reli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news