LONDON-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo kipindi cha miaka minne kwa mageuzi katika sekta mbalimbali na kuimarika kwa mifumo.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo katika Jukwaa la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu lililofanyika katika Makao makuu ya Ofisi za Citibank jijini London leo Aprili 8, 2025 na kuhudhuriwa na Kampuni mbalimbali za uwekezaji za Uingereza zenye nia ya kuchangamkia fursa za uwekezaji Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwepo kwa Citibank kuwa mshirika mkuu wa maendeleo Zanzibar kutachochea zaidi uwekezaji katika sekta za uchumi wa buluu, nishati , pamoja na nyumba na makaazi.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amesema ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma unalenga kuzifanya bandari kuwa za kisasa, uanzishwaji wa viwanda vya usindikaji wa mazao ya baharini.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito katika jukwaa hilo kuwekeza katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki, utalii wa mazingira, na uhifadhi wa baharini.