Ziara ya Rais Dkt.Mwinyi nchini Uingereza na faida tele kwa Zanzibar

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa, ziara yake Uingereza imekuwa na manufaa makubwa kwa Zanzibar, kwani wawekezaji wengi wameonesha dhamira ya kuwekeza nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Aprili 11,2025 alipozungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume,Zanzibar.

Ni baada ya kuwasili nchini akitokea Uingereza alikohudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Madola wa Masuala ya Biashara na Uwekezaji uliojikita katika Agenda ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema  Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kila mwaka ambapo sasa umefikia zaidi ya asilimia 7.
Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa, ukuaji huo wa uchumi utaendelea kukua zaidi kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuwa na sera bora na kuzitangaza fursa pamoja na kuwakaribisha wawekezaji zaidi wa mataifa mbalimbali kuwekeza nchini.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amezitaja sekta tatu kuu za uchumi ikiwemo Utalii,Uchumi wa Buluu na Utafutaji wa Mafuta na Gesi ndio Sekta za Kipaumbele kwa Serikali ambazo wawekezaji wengi wamedhamiria kuwekeza na Serikali imewahakikishia ushirikiano kufanikisha azma zao.

Amebainisha kuwa, wawekezaji wengi wa Uingereza wameonesha nia ya kuwekeza katika kuliongezea thamani zao la Mwani kwa kuongeza mnyororo wa thamani pamoja na uzalishaji wa mbegu bora,utafiti na kuwajengea uwezo wakulima wa mwani.
Akizungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi amesema, kampuni nyingi zimejitokeza ambazo zimeingia Mkataba na Serikali Juu ya Utafutaji wa Data za Mafuta na Gesi na Kuzitangaza Duniani kwa ajili ya kupata wawekezaji zaidi.

Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia wawekezaji kuwa, Zanzibar bado ina fursa nyingi za uwekezaji na kukuza uchumi na Serikali inazitangaza kwa kiwango kikubwa.

Kuhusiana na Nishati ya Umeme, Rais Dkt.Mwinyi amewakaribisha wawekezaji wa Uingereza kuwekeza nchini katika Umeme wa Upepo,Takataka na Jua ili kuiwezesha Zanzibar kujitegemea kwa nishati hiyo muhimu.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, nchi imeanza kuzidiwa na matumizi makubwa ya umeme hivi sasa hivyo uwekezaji katika eneo hilo lina umuhimu mkubwa.

Kwa upande wa Utalii amesema, Zanzibar inasisitiza Sera ya Utalii Endelevu na tayari imewaelimisha wawekezaji kuzingatia sera hiyo hususani uhifadhi wa mazingira na kwamba Zanzibar inahitaji watalii wenye uwezo watakaoifanya nchi kupata fedha nyingi na sio idadi kubwa ya watalii.
Akizungumzia suala la Wazanzibar wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) amesema,mchakato wa kuwapatia hadhi maalum umefikia pazuri,kwani tayari umewasilishwa bungeni ili kupata ridhaa ya Bunge hilo ili nao wapate fursa za msingi ikiwemo ununuzi wa ardhi,bima ya usafiri na kutambulika kwa familia zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news